1 Siku ya kwanza ya mwezi wa sita mwaka wa pili wa utawala wa mfalme Dario wa Persia, Mwenyezi-Mungu alimpa Hagai ujumbe aupeleke kwa Zerubabeli mwana wa Shealtieli, mkuu wa Yuda, na kuhani mkuu Yoshua mwana wa Yehosadaki.
2 Hagai akasema: “Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema hivi: Watu hawa wanasema kwamba wakati wa kulijenga upya hekalu langu haujafika.”
3 Lakini Mwenyezi-Mungu ameniambia mimi nabii Hagai,
4 “Je, ni sawa kwenu kukaa katika majumba yenu ya fahari hali hekalu langu ni magofu matupu?”
5 Sasa, asema hivi Mwenyezi-Mungu: “Fikirini kama mnafanya sawa!
6 Nyinyi mmepanda mbegu kwa wingi, lakini mmevuna kidogo; mnakula, lakini hamshibi; mnakunywa divai, lakini hamtosheki; mnavaa nguo, lakini bado mnasikia baridi; mfanyakazi mshahara wake huwa kama umetumbukizwa katika mfuko uliotoboka.”
7 Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema hivi: “Fikirini kama mnafanya sawa!
8 Sasa, basi, nendeni milimani mkalete miti, mlijenge upya hilo hekalu, nipate kulifurahia na kutukuzwa.
9 “Mlitazamia mavuno mengi, lakini mlipata kidogo tu. Na mlipoyaleta nyumbani, niliyapeperusha mbali. Kwa nini? Kwa sababu hekalu langu ni magofu matupu hali kila mmoja wenu anashughulikia nyumba yake.
10 Ndio maana mbingu zimeacha kunyesha mvua, nayo ardhi haioteshi mavuno.
11 Nimeleta ukame nchini, ukaathiri vilima na mashamba ya nafaka, mashamba ya mizabibu na mashamba ya mizeituni na kila mmea, watu na wanyama, na chochote mlichotolea jasho.”
12 Ndipo Zerubabeli mwana wa Shealtieli, na kuhani mkuu Yoshua mwana wa Yehosadaki, pamoja na watu wote waliokuwa wamerudi kutoka uhamishoni wakafanya kama Mwenyezi-Mungu, Mungu wao alivyowaambia na kama walivyoambiwa na nabii Hagai, kama alivyotumwa na Mwenyezi-Mungu, Mungu wao. Watu wakamcha Mwenyezi-Mungu.
13 Kisha Hagai, mjumbe wa Mwenyezi-Mungu, akawapa watu ujumbe ufuatao kutoka kwa Mwenyezi-Mungu: Mwenyezi-Mungu asema: “Mimi nipo pamoja nanyi.”
14 Basi, Mwenyezi-Mungu akawapa moyo Zerubabeli mkuu wa Yuda, kuhani mkuu Yoshua na watu wote waliokuwa wamerudi kutoka uhamishoni, walishughulikie hekalu. Walianza kazi hiyo ya kulijenga upya hekalu la Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wao,
15 mnamo siku ya ishirini na nne ya mwezi wa sita, mwaka wa pili wa utawala wa mfalme Dario.
1 Mnamo siku ya ishirini na moja, mwezi wa saba mwaka huohuo, neno la Mwenyezi-Mungu lilimjia nabii Hagai.
2 Alimwambia Hagai aongee na mkuu wa Yuda, Zerubabeli mwana wa Shealtieli, kuhani mkuu Yoshua mwana wa Yehosadaki na watu wote waliorudi kutoka uhamishoni awaambie hivi:
3 “Je, kuna yeyote kati yenu asiyekumbuka jinsi hekalu hili lilivyokuwa la fahari? Sasa mnalionaje? Bila shaka sasa mnaliona kama si kitu!
4 Hata hivyo, usife moyo, ewe Zerubabeli. Jipe moyo, kuhani mkuu Yoshua mwana wa Yehosadaki. Jipeni moyo nanyi watu wote wa nchi hii. Fanyeni kazi, maana mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi, nipo pamoja nanyi.
5 Mlipotoka Misri niliwaahidi kwamba daima nitakuwa pamoja nanyi. Basi, ningali pamoja nanyi, kwa hiyo, msiogope kitu.
6 “Naam, mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi nasema, hivi karibuni nitazitikisa mbingu na dunia, bahari na nchi kavu.
7 Nitayatikisa mataifa yote na hazina zao zote zitaletwa humu, nami nitalifanya hekalu hili kuwa la fahari. Mimi nimesema.
8 Fedha na dhahabu yote duniani ni mali yangu.
9 Hekalu jipya litakuwa lenye fahari zaidi kuliko lile la awali, na mahali hapo ndipo nitakapowapa watu wangu fanaka.” Asema Mwenyezi-Mungu wa majeshi.
10 Mnamo siku ya ishirini na nne ya mwezi wa tisa, katika mwaka wa pili wa utawala wa Dario, neno la Mwenyezi-Mungu wa majeshi lilimjia nabii Hagai,
11 akamwambia: “Waambie makuhani watoe uamuzi juu ya jambo hili:
12 Kama mtu akichukua nyama takatifu katika upindo wa vazi lake, kisha akagusa kwa upindo wa vazi hilo mkate au chakula kilichopikwa, au divai, au mafuta au chakula cha aina yoyote ile, je, chakula hicho kitakuwa kitakatifu?” Makuhani wakamjibu, “La, hasha.”
13 Hagai akawauliza tena, “Je, mtu aliye najisi kwa kugusa maiti, akigusa baadhi ya vyakula hivi, chakula hicho kitakuwa najisi?” Makuhani wakamjibu, “Ndiyo, kitakuwa najisi.”
14 Hapo Hagai akawaambia, “Mwenyezi-Mungu asema kwamba, hivyo ndivyo ilivyo kwa watu wa taifa hili na kila kitu wanachofanya; kadhalika na kila wanachotoa madhabahuni ni najisi.
15 “Lakini sasa angalieni mambo yatakayotukia. Kabla ya kuanza kujenga upya hekalu langu,
16 hali yenu ilikuwaje? Mliliendea fungu la nafaka mkitarajia kupata vipimo ishirini, lakini kulikuwa na vipimo kumi tu. Mliliendea pipa la divai mkitarajia kujaza vyombo hamsini, lakini mlikuta ishirini tu.
17 Niliwapiga kwa ukame, ukungu na mvua ya mawe, nikaharibu kila mlichojaribu kupanda, lakini hata hivyo hamkunirudia. Nasema mimi Mwenyezi-Mungu.
18 Leo ni siku ya ishirini na nne ya mwezi wa tisa, siku ambayo msingi wa hekalu umekamilika. Basi, ngojeni mwone yale yatakayotokea tangu leo.
19 Ingawa sasa hamna nafaka ghalani, nayo mizabibu, mitini, mikomamanga na mizeituni haijazaa kitu, lakini tangu leo, nitawabariki.”
20 Siku hiyohiyo ya ishirini na nne, mwezi wa tisa, neno la Mwenyezi-Mungu lilimjia Hagai mara ya pili:
21 “Ongea na Zerubabeli mkuu wa Yuda, umwambie hivi: Niko karibu kuzitikisa mbingu na dunia,
22 kuangusha falme na kukomesha nguvu zao. Nitayapindua magari yao ya farasi na wapandafarasi wake, nao wataanguka na kuuana wao kwa wao.
23 Siku hiyo, nitakuchukua wewe mtumishi wangu Zerubabeli mwana wa Shealtieli, na kukuteua ili utawale kwa jina langu. Wewe ndiwe niliyekuchagua.” Mwenyezi-Mungu wa majeshi amesema.